Mji wa Lagos, nchini Nigeria unaendelea kukumbwa na hali ya sintofahmu, baada ya vikosi vya usalama kuwatawanya kikatili vijana walioandamana dhidi ya ghasia za polisi, na kuua watu kadhaa kulingana na shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Amnesty International.
Wakazi wengi wamelazimika kujifungia nyumbani kwao huko Lagos, jiji na jimbo lenye watu milioni 20 ambapo sheria ya kutotoka nje, iliyotangazwa na kuanza kutumika tangu Jumanne jioni, muda wa sheria hiyo umeongezwa hadi saa 72.
Jana Jumatano visa vya uporaji na uharibifu mkubwa viliripotiwa katika maeneo kadhaa, ambapo barabara nyingi zilizuiliwa na vizuizi vilivyowekwa na magenge ya watu wenye hasira.
Rais wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amelaani vurugu zinazoendelea nchini Nigeria
Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kukomeshwa kile alichokiita “ukatili” wa polisi nchini Nigeria, ambayo imekumbwa na maandamano kwa wiki mbili sasa. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema katika taarifa kuwa Guterres amevihimiza vikosi vya usalama kujiuzia kwa wakati wote, wakati akitoa wito kwa waandamanaji kuandamana kwa amani na kujiepusha na machafuko.