Nigeria imesimamisha mtihani wa kitaifa unaoendelea kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho katika shule za sekondari kufuatia mapigano makali yanayoendelea baina ya waandamanaji dhidi ya polisi na vikosi vya usalama nchini humo.
Baraza la Mitihani la Taifa nchini humo (NECO) limesema uamuzi wa kusimamisha mitihani hiyo umetokana na amri ya kutotoka nje iliyowekwa na baadhi ya magavana wa majimbo.
Maeneo kadhaa katika jiji la Lagos yameathiriwa na machafuko hayo ikiwemo Kituo cha kibiashara cha Lagos, majengo kuteketezwa, vituo vya ununuzi kuporwa, magereza kushambuliwa pamoja waandamanaji na kupigwa risasi.
NECO imewaamuru wasimamizi wa mitihani kurudi kwenye vituo vyao na kusubiri maagizo zaidi, Afisa wa Baraza la Mitihani amesema mitihani hiyo itaanza tena katikati ya Novemba.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari aliwahimiza waandamanaji kuacha kuandamana na badala yake washirikiane na serikali “katika kutafuta suluhisho”.