Kampuni ya dawa ya nchini Marekani iitwayo Moderna imetangaza kuwa uchambuzi wa awali unaashiria kwamba chanjo yake inayoendelea kufanyiwa utafiti inaweza kuzuia ugonjwa wa COVID-19 kwa asilimia 94.5.
Mkuu wa kampuni hiyo Stephen Hoge ameyakaribisha mafanikio yaliyopatikana na kusema yanaleta matumaini kwamba chanjo dhidi ya virusi vya corona itasaidia kuzuia janga hilo na kurejea kwa maisha ya kawaida.
Matokeo hayo katika hatua muhimu ya majaribio ya maabara yanafanana na yale yaliyofikiwa na kampuni mbili za Pfizer na BioNTech ambazo zilitangaza kwa pamoja wiki iliyopita kuwa chanjo wanayoitengeza imepata mafanikio kwa asilimia 90.
Umoja wa Ulaya umesema tayari umeanzisha mazungumzo na kampuni ya Moderna ili kupata shehena ya dozi milioni 160 ya chanjo hiyo pindi itapatiwa ithibati.