Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu Mhandisi Baraka Mtunga (43) na Rajabu Katunda (42) kulipa faina ya Sh. Milioni 1.5 kwa kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kusambaza Huduma ya Internet bila kibali na kuisababishia hasara Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zaidi ya Sh. Milioni 200.
Pia washtakiwa hao, wametakiwa kulipa fidia ya Sh.Mil 267.656.794.30 baada ya kuingia makubaliano na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kutokana na kukiri kwao makosa hayo.
Washitakiwa hao wamefanikiwa kulipa kiasi cha Sh.Milioni 200 kati ya fedha hizo.
Hukumu hiyo, imetolewa ba Hakimu Mkazi Mkuu, Kassian Matembele baada ya kupokea makubaliano baina ya washtakiwa na DPP na kukiri makosa mawili ya kutumia mitandao kilaghai na kuisababishia hasara TCRA.
Hakimu Matembele alisema Mahakama imezingatia hoja za pande zote mbili, ambapo upande wa mashtaka uliomba adhabu kali itolewe na upande wa utetezi waliomba kupunguziwa adhabu kwa sababu washtakiwa wameonesha busara ya kukiri makosa yao.
Miongoni mwa mashitaka yaliyokuwa yakiwakabili ni kuisababishia mamlaka hasara ambapo wanadaiwa walilitenda kati ya Desemba 13, 2019 hadi Septemba 28, 2020 katika Hifadhi ya Taifa Saadani katika kijiji cha Kanjoo, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na maeneo mengine ya jiji la DSM ambapo waliisababishia TCRA hasara ya Sh.Mil 267.