Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Tabora imemuhukumu kifungo cha maisha aliyekuwa akifanyakazi ya kubeba abiria kwa njia ya baiskeli Mjini Tabora baada ya kukutwa na hatia ya kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka minne ambapo alipewa kazi na wazazi wa mtoto huyo ya kumpeleka shule na kumrejesha nyumbani.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 21 mkazi wa Tabora Mjini imedaiwa Mahakamani hapo na Wakili upande wa Jamhuri, Tito Mwakalinga kwamba mshtakiwa aliyefahamika kwa jina la Meshack Jame alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 154 Ibara ndogo ya kwanza na ya pili Julai 2, mwaka huu alipokuwa akimrudusha nyumbani mtoto huyo.
Katika maelezo hayo yaliyowasilishwa mahakamani na Wakili huyo katika shauri hilo la ukatili dhidi ya mtoto Namba 89/2020 likionesha madai ya kumlawiti mtoto huyo na kutolewa ushahidi na mashahidi watano akiwemo daktari ambao Mahakama imejiridhisha pasi na shaka kwamba kijana Meshack James alimfanyia ukatili huo wa kumlawiti mtoto huyo wa kiume akiwa nyumbani kwake na kisha kumtelekeza mtoto nje ya Geti.
Hakimu mkazi Mkoa wa Tabora, Jovin Kato ametoa hukumu hiyo akisema iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia chafu ambayo kimsingi haikubaliki katika jamii na kwamba inawadhalilisha watoto kwa ujumla.