Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), Biswalo Mganga ameeleza uamuzi wake wa kumfutia mashtaka kada wa CHADEMA, Nusrat Hanje ambaye Novemba 27, 2020 alivuliwa uanachama wa chama hicho pamoja na wenzake 18.
Nusrat ambaye alikuwa Katibu wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) alikaa mahabusu siku 163 na siku moja baada ya kutoka mahabusu jina lake lilikuwa miongoni mwa majina ya wanawake walioapishwa Novemba 24, 2020 mjini Dodoma kuwa Wabunge wa Viti Maalum.
Mbali na CHADEMA kupinga kuapishwa kwa wanawake hao kwa madai kuwa majina yao hayakupitishwa na kamati kuu ya chama hicho na kwamba kilichofanyika ni usaliti, pia walihoji kitendo cha Nusrat kutoka mahabusu na moja kwa moja kuapishwa wakati alipaswa kujaza fomu Novemba 20, 2020 na alitoka mahabusu wakati muda wa kujaza fomu hiyo ukiwa umepita.
Akizungumza na wanahabari katika gereza kuu la Karanga Mjini Moshi, Mganga amesema yeye ndio aliyemwachia kada huyo kutokana na mamlaka aliyonayo chini ya kifungu 91 cha CPA cha 2002.
DPP Mganga alitoa kauli hiyo wakati akitoa taarifa ya kuwafutia mashtaka watuhumiwa 72 ambao walikidhi sifa za kufutiwa mashtaka kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kubambikiwa makosa.
Mganga alimtaja mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kuwa yeye na wenzake angeweza kuwashtaki kama Nusrat lakini aliamua kufuta mpango huo kutokana na uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020.