Padre wa Kanisa Katoliki, Paroki ya Manushi, Jimbo la Moshi mkoani Kilimanjaro, Erasmus Swai, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Hai akituhumiwa kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa miaka 17 wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Kimaseki Arusha.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa kiroho kwa sasa amesimamishwa majukumu ya utumishi wa kanisa, hivyo kurudi kijijini kwake Msufini Uru, Wilayani Moshi Vijijini.
Padre Swai anayekabiliwa na kesi namba 159 ya Mwaka 2020 na alifikishwa mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Thurston Kombe na kusomewa mashtaka mawili.
Mashtaka hayo ni kubaka chini ya kifungu 130 cha Sheria ya 2002 na kumpa mwanafunzi ujauzito chini ya kifungu no. 60A cha sheria ya elimu.
Awali, ilidaiwa na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Lobulu Mbise, kuwa Machi, mwaka huu katika Hoteli ya Snow view katika Mji wa Boman’gombe wilayani Hai kwa nyakati tofauti, Padre Swai alimbaka mwanafunzi huyo.