Mfanyakazi wa TANESCO mkazi wa Kibaha kwa Mathias Mkoani Pwani amefikishwa katika mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam ikiwemo kosa la uhujumu kwakuingilia miundombinu ya umeme ya reli ya kisasa ya SGR nakuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi milioni sitini na mbili.
Kesi hiyo ya uhujumu namba 95 ya mwaka 2020 imesomwa na wakili wa Serikali Mkuu Martenus Marando mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama ya Kisutu Kassian Matembele ambaye amedai kuwa mshitakiwa Godfrey Maleko ametenda kosa hilo Mei 15,2018 maeneo ya TANESCO Majani ya Chai jijini Dar es Salam.
Wakili Marando amedai mshitakiwa Maleko aliiba nyaya hizo zenye urefu wa mita 403 ambazo zimetengwa kwa ajili mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR nakuisababishia Serikali kiasi kilichotajwa.
Baada ya kusomewa mashashitaka yanayomkabili mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote kwakuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Hata hivyo Wakili Marando amedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo akaomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa shauri hilo.
Baada ya kusikiliza hoja za upande wa Mashtaka Hakimu Matembele amehirisha kesi hiyo hadi Decemba 17 mwaka huu.