Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara ikamilishe utaratibu wa kuwa na bei kikomo ya saruji ili kuuwezesha kila mkoa kujua bidhaa hiyo inapaswa kuuzwa kwa bei gani kwa nia ya kuondoa upandishwaji holela unaofanywa na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo hii leo Desemba 7, 2020, wakati akizungumza na wakuu wa mikoa, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Maafisa Biashara wa mikoa, mawakala wa saruji walioko mikoani na wakurugenzi wa viwanda vya saruji, kikao ambacho kimefanyika kwa njia ya video.
“Mfano saruji inazalishwa Tanga au Dar es Salaam, halafu Morogoro inauzwa kwa Tsh 28,000, sasa Kigoma itauzwaje lazima kuwe na bei kikomo” Waziri Mkuu.
Aidha Waziri Mkuu meongeza kuwa suala hilo halihitaji kuundiwa bodi kwa sasa, kwani vyombo vya kusimamia biashara vipo, wizara husika ipo, hivyo amewataka wahusika wote wahakikishe wanasimamia suala hilo kikamilifu ili kuwawezesha wananchi kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu.