Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo Desemba 8, 2020 amekagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi za Ikulu Mkoani Dodoma na kuelezea kuridhishwa na kiwango na kasi ya ujenzi wa majengo ya ofisi hizo unaofanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Ujenzi wa Ofisi hizo ulioanza Februari 17, 2020 unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 3 ijayo na unafanywa kwa usanifu na muonekano sawa na Ofisi za Ikulu zilizopo Jijini Dar es Salaam.
Msimamizi wa ujenzi wa ofisi hizo, Luteni Kanali George William Nyisa amemueleza Rais Magufuli kuwa ujenzi huo utakamilika kwa wakati uliopangwa.
Akikagua majengo yanayojengwa, Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na uimara wa nguzo na kuta zinazojengwa na amesema ni fahari kubwa kwa Taifa kujenga ofisi yake ya Ikulu kwa kutumia Jeshi badala ya kutumia wakandarasi kutoka nje ya nchi.