Vikosi vya Usalama vimewaokoa karibu wanafunzi 350 wa kiume waliotekwa nyara na wanamgambo wa itikadi kali kaskazini mwa Nigeria na kupelekwa msituni.
Gavana wa Jimbo la Katsina Aminu Bello Masari amesema jumla ya wavulana 344 waliokuwa wanashikiliwa katika Msitu wa Rugu katika Jimbo jirani la Zamfara wameachiliwa huru.
Katika operesheni hiyo ya uokozi, Vikosi vya Usalama vililizingira eneo ambalo vijana hao walikuwa wanashikiliwa na vilikuwa vimepewa maagizo ya kutofyatua risasi hata moja.
Wavulana hao wamepelekwa katika jimbo la Katsina na kukabidhiwa familia zao baada ya kufanyiwa uchunguzi wa matibabu.
Kundi la Boko Haram chini ya kiongozi wake Abubakar Shekau lilidai kuhusika na utekaji nyara huo wa Ijumaa wiki iliyopita katika shule moja ya sekondari ya serikali katika mji wa Kankara, jimboni Katsina.
Via: DW Swahili