Baada ya kusota rumande kwa takribani mwaka mmoja, hatimaye Ofisa Programu wa Kituo cha (LHRC) Tito Magoti na mwenzake, Theodory Giyani (36), mtaalamu wa Mfumo wa Kompyuta wameachiwa huru baada ya kulipa fidia ya Sh.Mil 17.3.
Wawili hao wameachiwa huru baada ya kuhukumiwa kulipa fidia hiyo ya Sh. Milioni 17.3 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambayo iliwatia hatiani kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega, baada ya washtakiwa hao kukiri mashtaka yao kwa DPP.
Mbali na kulipa fidia, mahakama hiyo, imewahukumu adhabu ya kutotenda kosa lolote la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia leo.
Hakimu Mtega alisema, mahakama hiyo imewatia hatiani washtakiwa hao kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
“Washtakiwa mmetiwa hatiani kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa, hivyo mnatakiwa kulipa kiasi cha Sh 17, 354,535 kama fidia kwa Serikali “ Hakimu Mtega.
Wawili hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Desemba 24, 2019 ambapo walidaiwa kati ya Februari mosi na Desemba 17, 2019 jijini DSM na katika maeneo mbalimbali ya ndani ya nchi Tanzania, mshtakiwa Magoti, Giyani na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani,walishiriki makosa ya uhalifu wa kupanga kwa kumiliki programu za kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kufanya uhalifu na kupelekea kujipatia fedha kiasi cha Sh 17, 354,535.