Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania limemkuta na hatia Muuguzi Valentine Kinyanga wa kituo cha afya Mazwi ambaye alilalamikiwa kwa kosa la kumpiga vibao mama aliyefika kujifungua kituoni hapo mnamo Januari 5, mwaka huu 2021.
Akisoma hukumu hiyo mbele ya Wakili wa Serikali Fortunatus Mwandu, Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Abner Mathube alisema kuwa Baraza limemtia hatiani mlalalamikiwa chini ya kifungu 26(a)(c) ya sheria ya uuguzi na ukunga kwa kosa la kwanza na la pili.
Mathube alisema kuwa baraza lilichambua maelezo ya mlalamikiwa, mlalamikaji pamoja na mashahidi kuhusu kosa la kwanza la kumpiga mgonjwa kinyume na kifungu 25(3)(c)cha sheria ya uuguzi na ukunga Tanzania.
Katika kosa la kwanza lililotolewa ushahidi ulithibitisha kuwa ni kweli mlalamikiwa alimpiga mlalamikaji na mtuhumiwa alikiri kumpiga mlalamikaji
Aidha, kosa la pili lilikuwa ni kushindwa kusimamia maadili na weledi wa kitaaluma kinyume na kifungu 25(3)(k) lilithibitika kwa mtuhumiwa kushindwa kufuata utaratibu wa utoaji wa huduma za uuguzi na ukunga kwa mlalamikaji, kushindwa kuchukua na kuhifadhi taarifa za vipimo vya mgonjwa, kushindwa kufuatilia mwenendo wa uchungu wa mgonjwa wakati wa kumpokea katika kituo cha kutolea huduma na kuruhusu mtu ambaye sio mtaaluma kumpima mlalamikaji(mgonjwa)
“Kwa kuzingatia utetezi wa mlalamikiwa na ushahidi uliotolewa na mlalamikaji na mashahidi, umethibitisha mashitaka yote kama alivyo shatakiwa na mlalamikaji na kwa kuangalia uzito wa makosa yaliyobainishwa dhidi ya mlalamikaji ya kwamba angeweza kusababisha madhara makubwa kwa kumchapa vibao mama ambaye alikua tayari amejifungua pasipo msaada wake,Muuguzi huyo alipaswa kumuhudumia kwa kwa weledi na upendo mkubwa”.