Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo ameelekeza Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha Stendi Mpya ya Mabasi ya Mbezi Luis inaanza kutumika muda wowote kuanzia sasa baada ya kujiridhisha kukamilika kwa miundombinu yote muhimu kasoro barabara ya kuingia kituoni hapo ambayo ipo hatua ya mwisho.
Waziri Jafo amesema hayo wakati alipofanya ziara katika stendi hiyo ambapo amesema muda wowote ambao TANROAD watathibitisha kuwa barabara ya kuingia kituoni hapo imekamilika ni vyema kituo kikaanza kutoa huduma.
Aidha Waziri Jafo amesema kutokana na stendi hiyo kuwa na hadhi ya kimataifa anapendekeza ipewe jina la Rais Dk John Magufuli kama sehemu ya shukrani na kuthamini jitiada alizofanya ambapo amesema atamuomba Rais aridhie ombi hilo.