Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli ameipandisha hadhii Halmashauri ya Kahama Mji kuwa Manispaa ambapo sasa Kahama Mji itajulikana kama Manispaa ya Kahama.
Rais Magufuli pia amemsamehe Mkurugenzi wa Kahama Mji, Underson Msumba kutokana na kashfa ya kununua gari la kifahari ambapo amesema amemuachia gari hilo kutokana na jinsi anavyofanya kazi vizuri na kwa kujituma akishirikiana na Madiwani ambapo wamekuwa wakitekeleza miradi yenye kuwaletea maendeleo wananchi.
“Kahama panapendeza, nimekuta kiwanda kama vile vinavyojenga Ulaya, Mkurugenzi wa Kahama na Madiwani wana akili sana, wametoa eneo bure hawakumuuzia Mwekezaji, wameangalia mbele kwamba watatengeneza ajira na wataongeza kodi, ni busara kubwa sana” JPM
“Nikawa namuangalia Mkurugenzi alikuwa na tuhuma kidogo ya kujinunulia gari, nikapelekwa kwenye mradi wa tatu nikakuta kiwanda kikubwa kama nilivyokuwa naviona Ulaya nasema kwa dhati kwa sababu viwanda vinavyojengwa Ulaya ni kama hiki” JPM
“Huyu Mkurugenzi wa Kahama ana akili sana, alikuwa na makosa ya kujinunulia gari lakini leo nimekusamehe na gari nakurudishia ufanye kazi zako ila usijinunulie tena gari kinyume na utaratibu, najua unapigwa vita ila wanaokupiga vita kuanzia sasa wakuogope” JPM
“Nimetembelea Hospitali ya Wilaya ya Kahama ili kuweka jiwe la msingi ujenzi wa jengo la OPD, Kahama mko vizuri, kwakuwa leo nimeitangaza Kahama kuwa Manispaa, nawaongezea Milioni 500 ili Hospitali ile iboreshwe na kuwa yenye hadhi ya Manispaa,” JPM