Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Mabula Mchembe amewataka Wananchi kupuuza taarifa zinazozagaa kupitia mitandao ya kijamii juu ya uwepo wa wagonjwa wa corona katika Mkoa wa Dar es Salaam na wamelazwa hospitali ya Muhimbili na Mloganzila, na kusisitiza kuwa sio kila tatizo la mfumo wa upumuaji ni ugonjwa wa corona.
Prof. Mchembe amesisitiza hilo leo wakati alipofanya ziara katika Hospitali ya Mloganzila na Muhimbili ili kujua ukweli juu ya taarifa hizo, na kubaini kuwa taarifa hizo sio sahihi na zinapaswa zipuuzwe ili kuondoa hofu kwa wananchi.
“Nimeweza kupita Hospitali ya Mloganzila na pia nimepita hapa Muhimbili, kuweza kukutana na wafanyakazi ili kuongea nao pia kusikia changamoto wanazopata, tumeweza kupita kwenye wodi ili kuona matatizo yaliyopo na kuona wagonjwa waliopo na kujiridhisha kwamba sio kila wagonjwa waliolazwa Hospitali wana ugonjwa wa Corona kama ambavyo inasemekana kwenye mitandao,” Prof. Mchembe.
Ameongeza kuwa, kuna wagonjwa waliolazwa wana matatizo ya kupungukiwa damu, wapo waliolazwa wana matatizo ya mfumo wa kupumua, kuna wengine wamelazwa wana matatizo ya ajali, wengine matatizo ya kuanguja(kifafa), wengine wa seli mundu na hata wengine wana Athma, lakini wote hawa ukijumlisha dalili zao za ugonjwa zinaweza kufanana, wapo wanaoumwa kichwa, wapo wenye mafua, mwingine anashindwa kupumua kutegemea na mwili wake.
Aidha, Prof. Mchembe ameweka wazi kuwa, hali ya kufanya kazi ya Watumishi katika kutoa huduma kwenye Hospitali hizo ipo juu, huku wakiendelea kuwahudumia wagonjwa wote kama kawaida bila hofu yoyote na wala bila kuvaa mavazi yoyote ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Corona.