Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameipa siku mbili Wizara ya TAMISEMI kufuatilia Halmashauri za Wilaya ambazo zilikuwa na makao makuu yake katika Halmshauri za Miji, kuhakikisha zinahamia kwenye makao mapya na zisipotekeleza apelekewe taarifa ofisini kwake Jumamosi Februari 6 saa 4 asubuhi.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Februari 4, 2021, Bungeni Dodoma, katika kikao cha tatu, mkutano wa Pili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali la mbunge wa Geita vijijini Joseph Musukuma, aliyehoji ni hatua gani zitachukuliwa kwa halmashauri ambazo zimekaidi agizo la Rais Magufuli, kwani wafanyakazi wake wanakwenda kulala mijini na kwamba wanazidi kuongeza gharama kwa serikali.
“Ni kweli Rais alitoa agizo na halmashauri nyingi zililitekeleza, nataka niagize halmshauri zilizotakiwa kuhama waondoke mara moja na wasipofanya hivyo mkuu wa mkoa husika achukue hatua dhidi ya watu hao ambao hawataki kwenda kwenye maeneo mapya” Waziri Mkuu
“Naiagiza pia TAMISEMI kufuatilia kila halmshauri ambayo ilitakiwa kuhama na nitahitaji taarifa hizo Jumamosi ofisini kwangu saa 4:00 asubuhi ili nijue ni halmashauri gani watumishi hawajahama ili tuchukue hatua za kinidhamu kwa watumishi hao” Waziri Mkuu