Watumishi kumi na moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera wamepabdishwa kizimbani kujibu mashtaka ya wizi wa zaidi ya Sh400 Milioni.
Mbele ya Mahakimu watatu tofauti, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dominick Maganga amedai kwa nyakati tofauti, washtakiwa hao walifanya ubadhirifu wa fedha hizo walizokuwa wakikusanya kupitia mashine za kielektroniki za kukusanyia kodi.
Kwa nyakati tofauti, washtakiwa hao walisomewa mashtaka mbele ya mahakimu Flavian Kubingwa, Christian Rugumila na Subira Mashambu.
Washtakiwa wanaodaiwa kuwa kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2018 na June 2020 walikusanya fedha hizo bila kuziwasilisha Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Biharamulo.
Miongoni mwa waliofikishwa Mahakamani ni Mhasibu wa mapato wa Halmashauri hiyo, Salanga Mahendeka na Theresa Nicodem ambaye ni Ofisa Afya Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo.
Wengine wanaokabiliwa na mashtaka ni Jeremiah Kasaizi, Revocatus Mwesiga, Allen Rwiza, Godeliva Karantin, Christian Magorwa, Allen Rwiza, Shakiru Sued, James Ndibwire, Gilimon Msengi na Joyce Nkuba.
Watuhimiwa wote walikana mashtaka dhidi yao ambapo 10 kati yao walipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kusaini hati ya dhamana ya Sh10 milioni au kuweka mahakamani fedha taslimu inayolingana na nusu ya fedha hizo au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya nusu ya fedha wanayodaiwa kuiba.
Wakati wenzake wakipelekwa mahabusu hadi Februari 15, 16 na 17, 2021 mashauri yao yatakapotajwa, mshtakiwa Allen Rwiza aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.