Mshitakiwa wa Kwanza, Sadikiel Meta (71) aliyekabiliwa na kesi ya Biashara haramu ya Kusafirisha Binadamu ikiwemo (kutumikisha Walemavu) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu amefariki Dunia.
Mzee Sadikiel na wenzake 13 walifikishwa mahakamani hapo January 13, 2021 wanakabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi yenye mashitaka 41 ikiwemo kutumikisha Walemavu.
Taarifa ya kifo cha mshtakiwa huyo imetolewa leo na Wakili wa Utetezi, Robert Langeni mbele ya hakimu mkazi mkuu, Kassian Matembele wakati kesi hiyo ilipoitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili huyo amesema mshtakiwa Meta aliugua akiwa gerezani na kupelekwa katika Hospitali ya wilaya ya Temeke kwa matibabu lakini Januari 28, 2021 akafariki dunia.
Aliieleza mahakama hiyo kuwa Meta alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa Kisukari na tayari mazishi yalishafanyika wiki iliyopita mkoani Moshi, Kilimanjaro.
Upande wa wakili wa Serikali, Kija Luzungana ameieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Matembele baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 23, mwaka huu itakapo tajwa.
Hata hivyo Leo kesi hiyo imeendeshwa kwa mfumo wa Digitali yaani kwa njia ya video ambapo ambao washtakiwa wote wapo Segerea.
Washtakiwa waliobakia ni Yusuph Mohamed (35), Yusuph Magadu (20), Emmanuel Salu (20) Gogad Mayenga (18), Samson Taruse (26), Hussein John (18), Zacharia Paul (18), Dotto Shigula (19), Petro Simon (21), Emmanuel Sahani (38), Joseph Mathias (20), Masanja Paul (21), Aminiel Sangu (19), na Emmanuel Lusinge.
Miongoni mwa mashtaka yaliyomkabili Meta anadaiwa alishindwa kulipa kodi ya thamani ya Sh. Mil. 31,328,500.31 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) .
Pia mshtakiwa Meta alidaiwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. Milioni 31.3.
Katika shtaka la mwisho la utakatishaji imedaiwa kati ya Agosti 2020 na Januari Mosi 2021, mshtakiwa Meta alijipatia Sh. Milioni 31,328,500.31 huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kushindwa kulipa kodi.