Baraza la Seneti lilipiga kura 56 kwa 44 za kuendelea na kesi dhidi ya Trump, likizipinga hoja za mawakili wake kwamba Rais hawezi kushtakiwa pindi anapomaliza muda wake.
Maseneta ambao waliapishwa kama wazee wa baraza, walipitia picha za vidio za wafuasi wa Trump wakipambana na polisi, kuvamia kumbi za bunge na kupeperusha bendera za Trump.
Pia kuliwasilishwa vidio za Trump mwenyewe akiwahimiza wafuasi wake kabla ya uvamizi kuwa wapambane hadi tone la mwisho kupinga kushindwa kwake kwenye uchaguzi wa Novemba 3.
Kiongozi Mkuu wa mashtaka hayo Jammie Raskin aliwaeleza maseneta kwamba kesi hiyo itawasilisha “ukweli mgumu” dhidi ya Trump.
“Rais Trump ametuma mawakili wake hapa leo kujaribu kuzuia Bunge la Seneti kusikia ukweli wa kesi hii. Wanataka kuzima kesi kabla hata ya ushahidi wowote kutolewa. Hoja yao ni kwamba ikiwa unafanya makosa ya kushitakiwa katika wiki zako za mwisho mamlakani, basi unafanya ukiwa na kinga ya kikatiba na unanusurika”.