Magari ya kivita yametanda katika mitaa ya miji kadhaa nchini Myanmar huku kukiwa na ishara kwamba wanajeshi wanaandaa msako dhidi ya wale wanaopinga mapinduzi yaliyofanywa Februari 1.
Mtandao wa interneti umezimwa nchi nzima licha ya juhudi za kimataifa kupinga hatua hiyo.
Katika jimbo la kaskazini la Kachin, vikosi vya usalama vimefyatua risasi katika siku ya tisa ya maandamano ya kupinga mapinduzi nchini kote.
Afisa wa maalum wa umoja wa mataifa nchini humo amewashutumu wanajeshi kwa kile walichokiita kutangaza vita dhidi ya raia wasio na hatia.
Tom Andrews, mwandishi maalum wa umoja wa mataifa kuhusu Myanmar inayojulikana pia kama Burma, amesema majenerali walikuwa wakionesha dalili za kukata tamaa na kuwajibika.
Balozi mbalimbali za nchi za Magharibi zimehimiza jeshi kuonesha weledi wake wakati huu ambapo nchi hiyo ipo katika wakati mgumu.