Maafisa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamesema zaidi ya watu 60 wamezama baada ya mashua waliyokuwa wakisafiria kupinduka na kuzama katika mto Congo.
Watu 300 wameokolewa lakini inakisiwa kuwa watu wengine 200 hawajulikani walipo baada ya ajali hiyo.
Wakazi wanasema boti iligonga mwamba mashariki mwa mji mkuu Kinshasa, wakati walipokuwa wakisafiri usiku, safari za majini nyakati za usiku zimepigwa marufuku nchini humo.
Waziri wa Masuala ya Kibinadamu, Steve Mbikayi, ametaka wale wamiliki wa boti kushtakiwa.
“Chombo kilichojaa kupita kiasi, kilichokuwa na abiria zaidi ya 700 kilipinduka Mai-Ndombe! miili 60 tayari imepatikana na watu 300 wamenusurika tunatoa pole kwa familia zilizofiwa na tunataka hatua zichukuliwa dhidi ya wale wote wanaohusika na sekta ya uchukuzi,” aliandika Waziri huyo kwenye mtandao wa Twitter.