Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) kwa ushirikiano na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) pamoja na Chama cha Wahasibu Wanawake Tanzania (TAWCA) tunawakaribisha watanzania wote kwenye maadhimisho ya kila mwaka ya “Wiki ya Uhasibu”.
Wiki ya Uhasibu mwaka huu itaadhimishwa Machi 15 – 20, 2021 Jijini Dar es Salaam yakiwa na kaulimbiu inayosema: “Tunaunganisha Nguvu za Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu ili kuwatumikia Wananchi kwa Ustawi Bora wa Baadaye wa Taifa Letu” .
Kaulimbiu hii inaakisi ukweli kwamba kila mtu anautumia Uhasibu muda wote na mahali popote, katika mazingira yoyote katika hali yoyote kila mtu anahitaji kutumia kanuni za Uhasibu; ni vile tu wengine hawajui kama wanahitaji uhasibu katika maisha yao ya kila siku.
Watu wanaojua kwamba wanahitaji Uhasibu na wakafikia kujua kwamba wanamhitaji Mhasibu basi watu hao wamefanikiwa sana katika maisha yao na wanaweza kuthibitisha mafanikio yao tofauti na walipokuwa hawajatambua thamani ya Uhasibu.
Kusudi la maadhimisho haya ni kuwaleta pamoja watu wote kusherehekea, kufanya kumbukizi na kutambua kazi ya uhasibu na wahasibu ambao wanafanya kazi katika taasisi za aina zote na kwenye ngazi mbalimbali za majukumu. Wahasibu wanafanya kazi yenye kuchosha akili na yenye changamoto kubwa ya kuhakikisha rasilimali fedha na mikakati ya kifedha ya taasisi hizo inastawi katika mazingira ya sasa ya biashara.
Wahasibu ambao, ili kutimiza mahitaji haya ya biashara na ya kijamii, wanajikuta katika changamoto na shinikizo kubwa la kutengeneza taasisi zinazoweza kushindana, baadhi ya shughuli zitakazofanyika kwenye wiki hiyo ya uhasibu ni pamoja na: Kujengeana uwezo (Mentorship) ambapo tunakusudia kuwapandisha ngazi wahasibu kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine ya juu zaidi.
Kuanzisha taasisi au makampuni ya Uhasibu, Ukaguzi na Ushauri, watapata fursa kukutana na wenye Makampuni na ambao wameshabobea katika masuala ya Uhasibu. Aidha yatakuwepo Mashindano ya Michezo mbalimbali; Huduma kwa Jamii kama vile kutoa elimu na ushauri wa kibiashara kwa wafanyabiashara wa Kariakoo, kutoa kadi za bima ya afya kwa watoto yatima, kutoa msaada kwa wasioona, nk. Pia tutatoa Ushauri wa Kibiashara, Ushauri wa Ujasiriamali kwa Wanawake.
Hii ni nafasi nyingine kwa Umma wa Watanzania kuifahamu taaluma ya uhasibu na mchango wake kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu lakini pia kwa maendeleo binafsi ya kila mwanajamii mtanzania.
Ni nafasi kwa Wajasiriamali, Wafanyabiashara, Wafanyakazi, Wakulima, Wafugaji Wavuvi na taasisi mbalimbali za kibiashara na za huduma, kukutana na wahasibu na kupata ushauri wa kitaaluma. Ni nafasi ya umma kuchangamana na wahasibu na kufurahia kazi yao na umuhimu wake kwa maendeleo ya jamii yetu.
Chama Cha Wahasibu Tanzania (TAA) kwa pamoja na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu nchini (NBAA) na Chama cha Wahasibu Wanawake nchini (TAWCA) tunawaalika Wahasibu wote na Umma kwa ujumla kushiriki tukio hili na kuikuza taaluma hii adhimu. Tunawakaribisha pia wadau mbalimbali ambao wako tayari kudhamini maadhimisho haya kwa faida ya umma wa Watanzania wote.