Waasi wa Kihutu kutoka Rwanda FDLR, wamekanusha madai yanayowahusisha na mauaji ya balozi wa Italia nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na badala yake waasi hao wamewatuhumu wanajeshi wa Kongo na Rwanda.
Wizara ya mambo ya ndani ya Kongo iliwabebesha lawama waasi hao wa FDLR ya mauaji hayo ya balozi Luca Attanasio yaliyotokea jana Jumatatu baada ya msafara wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP kushambuliwa karibu na mji wa mashariki mwa nchi hiyo wa Goma.
Kwa mujibu wa duru za kidiplomasia mjini Kinshasa na shirika la WFP balozi huyo aliuwawa akiwa katika shughuli zake za kikazi katika eneo hilo.
Hata hivyo leo kundi hilo la waasi wa Kihutu kutoka Rwanda limetoa taarifa likidai kwamba msafara wa balozi ulishambuliwa karibu na mpaka wa Rwanda katika eneo ambalo sio mbali na ngome ya vikosi vya wanajeshi wa DRC na Rwanda.
Pia waasi hao wameitaka serikali ya Kongo na ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCO kuchunguza mauaji hayo badala ya kutowa shutuma.