M-Net, kampuni tanzu ya MultiChoice, ambayo kwa zaidi ya miaka 30 imejizolea umaarufu mkubwa kwa vipindi vyake vya burudani hususan filamu, imetangaza neema kwa tasnia ya filamu Tanzania ambapo imeanza kuitisha proposals kutoka kwa wazalishaji kwa ajili ya ufadhili wa filamu za kitanzania.
Kwa mujibu wa M-Net, sasa imeanza kupokea mapendekezo kutoka kwa wazalishaji wa filamu hapa nchini kwa ajili ya kufadhili uzalishaji wa filamu hizo ambazo zitatumiwa na M-Net kwenye chaneli zake ambapo kwa sasa M-Net ina chaneli 6 zilizopo Afrika Mashariki zinazoonyeshwa katika kisimbuzi cha DStv.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu ufadhili huo, Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania Ronald Shelukindo amesema kuwa kuanzia sasa hadi tarehe 14 Machi 2021, M-Net itakuwa ikipokea proposals kutoka kwa wazalishaji wa filamu za wa hapa nchini na hatimaye itayapitia mapendekezo hayo na hatimaye kuchagua filamu ambazo zitapata ufadhili huo.
Serikali, kupitia Bodi ya Filamu, imepongeza uamuzi huo wa M-Net na kuwataka wazalishaji wa kitanzania kuchangamkia fursa hiyo adhimu na kuhakikisha kuwa wanapeleka mapendekezo ya viwango vya juu kwani huu ni ulingo muhimu wa kutangaza na kupanua soko la filamu zetu za kitanzania.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dr. Kiagho Kilonzo, amesema hii ni fursa kubwa na Bodi yake imejipanga kutoa kwa kushirikiana na mashirikisho yote ya filamu hapa nchini kuhakikisha kuwa wazalishaji wetu wanaitumia fursa hii vizuri na kuahkikisha kuwa haki na maslahi yao na wasanii wetu yanazingatiwa.
Kwa muda mrefu sasa M-net imekuwa ikitumia filamu za kitanzania na kama mnavyokumbuka miaka minne iliyopita M-Net ilianzisha chaneli mahsusi kwa maudhui ya Kitanzania inayofahamika kama Maisha Magic Bongo.
Hivi sasa imekuja na mpango mkubwa zaidi mahususi weney lengo la kupata fiamu nyingi zaidi za kitanzania na sasa wazalishaji wetu wanatakiwa wachangamkie fursa hii adhimu kwani kama mnavyofahamu, chaneli za M-Net zinazorushwa kupitia DStv huonekana katika nchi mbalimbali duniani.
Mkuu wa masoko wa MultiChoice Tanzania amebainisha; “MNet imeaua kufadhili filamu halisi za Kitanzania zinazoakisi mila na desturi za kitanzania huku zikibeba maudhui mbalimbali ikiwemo maisha ya kila siku, mapenzi, mahusiano na kadhalika ilimradi tu yawe yanaakisi uhalisia na utamaduni wa Kitanzania”
Amesema filamu inatakiwa kuwa katika lugha ya Kiswahili au Kiingereza. Kwa zile za Kiswahili, itapaswa kuwa na tafsiri ya kiingereza (subtitle). Simulizi inatakiwa kuwa yakusisimua na kumfanya mtazamaji kuwa na hamu na shauku ya kusubiria awamu nyingine.
Mahitaji yanayopendekezwa ni pamoja na kulenga watazamaji wa umri kati ya miaka 20 hadi 45, muda- dakika 90 na iwe kwa Kiswahili au Kiingereza. Pia mzalishaji anapaswa kuwasilisha muongozo wa filamu, wasanii watakaocheza, majina kamili ya timu ya waandaaji, bajeti ya awali, sampuli ya kazi yoyote ya awali iliyofanywa na muombaji na pia stakabadhi ya kimkataba, ikielezea majina kamili ya kampuni, waongozaji, wadau, vielelezo vya usajili wa kampuni, hati za usajili mamlaka ya Mapato TRA na anuani kamili.
Wazalishaji wanaowasilisha mapendelezo yao wayawasilishe kwa njia ya barua pepe ambapo mwisho wa kupokea mapendekezo ni tarehe 14 Machi 2021.
Baada ya kupokelewa na kukaguliwa, mapendekezo atakayokidhi vigezo yatapitiwa na jopo na jopo la majaji watakaochaguliwa na wakuu wa chaneli ambao watatahini mapendekezo yaliyokidhi vigezo na kisha kuchagua mapendekezo yatakayoshinda.
Kwa mapendekezo yatakayoshinda, wazalishaji watapata ufadhili kamili (yaani wa gharama zote za uzalishaji) kutoka M-Net na katika mikataba hyo, viwango vya kitaalam na uhariri vinavyotakiwa na M-Net vitakuwa sehemu ya mkataba huo. Pia M-Net ndio watafanya uhariri wa mwisho na udhibiti wa ubunifu kulingana na matarajio ya filamu inayotakiwa.