Chama cha mawakili Tanganyika (TLS) kimepata pigo baada ya aliyekuwa mwanachama cha Chama hicho wakili Loomu Ojare kufariki dunia ghafla akiwa kazini
Mwenyekiti wa chama cha mawakili wa kujitegemea Kanda ya Arusha Elibariki Maeda akiiwakilisha TLS katika ibada ya kumuaga Ojare alisema kifo cha Ojare ni pigo kwa Chama na wanachama kwa ujumla
Maeda alisema Ojare alikuwa mchapakazi na mwenye kujituma ikiwemo kuwasaidia watu waliohitaji msaada wa kisheria bure kwa kuwa hakupenda kuona mtu akionewa
“Sisi kama mawakili tuliomkuta Ojare Kazini tulijifunza mambo mengi kutoka kwake alituelekeza pasipo kuchoka na alikuwa mtu aliyependa haki”alifafanua Maeda
Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Mahakama kuu Kanda ya Arusha John Nkwabi akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya serikali alisema Marehemu Ojare alikuwa akilea na kuwafundisha vijana wengi kwenye taaluma ya Sheria hivyo kuondoka kwake ni pigo kwa serikali na Taifa kwa ujumla
Nkwabi alisema Marehemu Ojare alikuwa mtu aliyependa haki na hakutaka kumwona mtu akidhulumiwa haki yake na kuwataka mawakili waliobaki kuiga Mfano wa Marehemu kwa kuendeleza kazi nzuri iliyoachwa na Ojare
Mchungaji kiongozi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Elkyurei Daniel Thimothi akiongoza ibada ya mazishi ya Marehemu Ojare alisema kuondoka kwa Ojare ni pigo si tu kwa jamii inayozunguka ila pia kwa kanisa hilo kwani alikuwa kiongozi wa Kanisa
“Marehemu alikuwa kiongozi wa kanisa na ujenzi wa kanisa hili yeye alikuwa wanakamati katika kamati ya ujenzi hivyo kanisa limepata pigo kubwa”Alisema Mchungaji Thimothi.
Awali akisoma risala ya Marehemu mtoto wa marehemu Diana Ojare alisema marehemu baba yake alifariki ghafla kwa kuwa hakuumwa kwa muda mrefu na kwamba siku ya kufariki marehemu Ojare alikuwa ofisini akihudumia wateja na baadae alijisikia vibaya na alipokimbizwa hospitali alifariki dunia
Diana alisema wao kama Familia kifo cha baba yao kimewaachia pengo kubwa kwa kuwa alikuwa msaada mkubwa kwao na tegemezi Kwa familia na hivyo kutoa shukrani kwa watu wote walioshiriki katika kumpumzisha baba yao
Marehemu Loomu Ojare alizaliwa mwaka 1952 na alifanya kazi kama wakili wa serikali kwa kipindi kirefu kabla ya kuachana na kazi za serikali na kujiajiri kama wakili wa kujitegemea mwaka 1983
Aidha Marehemu ameshiriki katika kazi mbalimbali za uwakili ambapo hadi umauti unamkuta alikuwa mwanachama wa chama cha mawakili Tanganyika (TLS) na mwanachama wa Club ya mawakili Arusha na ameacha watoto wanne.