Ripoti ya pamoja ya Shirika la Afya duniani WHO na China kuhusu chanzo cha mlipuko wa COVID-19, inaonyesha kwamba maambukizi kutoka kwa popo kwenda kwa binadamu huenda yalipita kwa mnyama mwingine na sio kutoka maabara.
Utafiti huo hata hivyo umetoa mwangaza kidogo wa jinsi gani mlipuko huo ulianza na unaacha maswali mengi bila ya majibu, lakini ripoti hiyo imetoa maelezo ya kina kwanini watafiti wamefikia hitimisho hilo.
Timu ya watafuti imependekeza utafiti zaidi katika kila eneo kasoro katika nadharia ya kwamba virusi hivyo vilianzia maabara, dhana ambayo iliwahi kuelezwa na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kuwa miongoni mwa sababu za mlipuko wa virusi vya corona.
Pia inasema kwamba dhana ya virusi hivyo kusambaa kupitia soko la vyakula vya baharini katika mji wa Wuhan China ambako kisa cha kwanza kiligundulika, haikuwa na uwezekano mkubwa.
Ripoti hiyo ambayo inatarajiwa kuwekwa hadharani hii leo, inatazamwa kwa ukaribu na wanasayansi wanaojaribu kufahamu chanzo cha mlipuko wa COVID-19 ili kuweza kuzuia magonjwa ya milipuko ya baadae, lakini pia imekuwa nyeti kwa China ambayo inadai kuwa haipaswi kulaumiwa kwa mlipuko huo.