Serikali imeahidi kuchukua hatua kali kwa mfanyabiashara yoyote atakaebainika kupandisha bei za bidhaa au huduma kwa utashi ama tamaa bila ya kuwepo sababu ya msingi kwani tayari imeshatoa bei elekezi za bidhaa muhimu za chakula.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema hayo katika risala yake aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ya kuukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhan mwaka huu 2021 Miladia sawa na mwaka 1442 Hijria.
Katika risala yake hiyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba kwa pamoja ni vyema wananchi wenye kipato cha chini wakafikiriwa hasa katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo mahitaji ya familia yanaongezeka.
Alisisitiza kwamba kwa msingi huo huo, wafanyabiashara wa bidhaa zote zikiwemo za nguo ni vyema wakazingatia uwezo wa wananchi kwani kuwakatia nguo watoto katika kipindi hichi kwa ajili ya Sikukuu ni sehemu ya utamaduni wa wananchi wote wa Zanzibar.
Aliongeza kuwa inafurahisha kuona kwamba licha ya kuwepo kwa changamoto za usafirishaji na upatikanaji wa biadhaa mbali mbali, shughuli za biashara na upatikanaji wa chakula hapa nchini zinaenda vizuri ambapo bidhaa zote muhimu zinapatikana wakati huu mwezi wa Ramadhani ukikaribishwa.