Inawezekana usiamini kwamba kuna sehemu zinagharimu zaidi ya shilingi Milioni 22 za Kitanzania kulala kwa usiku mmoja tu! amini au usiamini sehemu hizo zipo, tena hapa hapa nchini kwetu Tanzania.
Thanda, ni sehemu kwa ajili ya mapumziko iliyotengenezwa na mtu binafsi katika eneo la kisiwa cha Shungimbili kilichomo Wilaya ya Kisiwa cha Mafia. Kisiwa hiki kina ukubwa wa takribani hekari 20 ambamo ndani yake imejengwa nyumba moja.
Nyumba hiyo ina vyumba vya kulala vitano na vibanda viwili pembezoni mwa ufukwe wa bahari ya Hindi kusini mwa Tanzania ambapo familia ya watu mpaka 10 inaweza kuishi.
Ili kuweza kuishi kwenye kisiwa hiki, wamiliki hutoza wageni kiasi cha dola za kimarekani 10,000 kwa usiku mmoja ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 22 za kitanzania.
Mazingira ya kuvutia, utulivu wa hali ya juu na namna eneo hili lilivyotengenezwa ndivyo vinavyowafanya watalii kulipia gharama hizo na lisiwe ni jambo la kushangaza.
Ni jambo la kawaida ukiwa mapumzikoni kisiwani humo kuwaona au kuogelea pamoja na viumbe wa baharini kama vile pomboo (dolphin), papa wakubwa (whale sharks) na kobe wa majini.
Wamiliki wa Kisiwa hiki binafsi cha mapumziko, wanandoa Bw. Dan na Bi. Christin Olofsson ambao asili yao ni Sweden walipata wazo la kutengeneza sehemu hii ikiwa ni kwa ajili ya kupumzikia pamoja na watoto wao watatu na wajukuu nane.
Kikubwa kilichowasukuma kufanya hivyo ni katika jitihada za kubadili mazingira hususani hali ya hewa ukizingatia nchi za Scandinavia wanapotea hukumbwa na baridi kali kwa vipindi virefu vya majira ya mwaka. Walianza kwa kuwekeza Afrika ya Kusini kutokana na kuvutiwa na wanyama na uoto wa asili kabla ya kuja nchini Tanzania.