Aliyekuwa Afisa wa Polisi mjini Minneapolis Marekeni Derek Chauvin, amekutwa na hatia ya kumuua George Floyd.
Mahakama imemtia hatiani bwana Derek kwa mauaji hayo aliyoyafanya Mei 2020 kwa kumkandamiza na goti shingoni alipokuwa akimkamata.
Kaka wa Floyd, Philonise Floyd, amesema ni siku ya furaha kwa familia, taifa na watu weusi.
Baada ya Derek Chauvin kukutwa na hatia, sasa atasalia kizuizini hadi atakapohukumiwa na huenda akafungwa jela kwa miongo kadhaa.
Kwa upande wa Rais wa Marekani Joe Biden amesema hatimaye haki imetendeka. “Tutaongeza juhudi kuhakikisha mengine yanafikiwa. Hii itakuwa hatua ya kwanza muhimu ya kukabiliana na ubaguzi wa rangi uliokithiri katika mifumo yetu.”
George Floyd aliyefariki akiwa na umri wa miaka 46 alinunua pakiti ya sigara katika duka moja huko Minneapolis Kusini jioni ya tarehe 25 Mei 2020, akadaiwa kutoa pesa bandia na mwenye duka akapiga simu polisi na ndipo wakampiga katika makabiliano.