Wizara ya Afya imetoa maagizo 10 ya tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya corona ikiwemo kutumia sanitaiza, kunawa mikono na kuvaa barakoa.
Maagizo hayo yametolewa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Abel Makubi kupitia taarifa yake ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa hatua za kujikinga na magonjwa mbalimbali.
Prof. Makubi amesema wananchi wanatakiwa kuondoa hofu na kufuata hatua muhimu huku wakijifunza kuendelea kuishi na ugonjwa huo.
“Tuendeleze na tabia ya kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni, iwapo hakuna tumia vipukusi ‘sanitaiza’ na vaa barakoa pale panapolazimika,” Makubi
Amewataka Watanzania kuhakikisha wanafanya mazoezi, wanapata lishe bora ili kuwa na kinga za mwili za kutosha bila kusahau tiba za asili za kujifukiza na kunywa zile zilizodhibitishwa na baraza la tiba asilimia.
“Tambua afya yako, jilinde tukulinde. Wito huu unawahusu makundi maalum wakiwemo wenye uzito mkubwa, wazee, wenye magonjwa mbalimbali sugu ya muda mrefu kama pumu, shinikizo la juu la damu, kisukari magonjwa ya ini, figo, moyo nasi tutaendelea kuimarisha huduma za wazee na kliniki za magonjwa sugu,” Profesa Makubi
Amesisitiza wananchi kuwahi katika vituo vya kutoa huduma za afya na kutoa wito kwa maofisa afya wanaotoa huduma mipakani kuendelea kuimarisha udhibiti wa magonjwa kama miongozo inavyoelekeza.
Aidha amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ili waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya corona.