Watu 59 wamekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali ya jinai, ikiwemo kupatikana na dawa za kulevya aina ya Heroin gramu 1.25, mirungi kilo 456, misokoto 1,401 ya bangi na bastola moja iliyokuwa ikimilikiwa kinyume cha sheria.
Akiongea na Waandishi wa habari Kituo cha Polisi Himo, RPC wa Kilimanjaro, Amon Kakwale amesema watu hao walikamatwa katika operesheni na misako iliyoendeshwa na jeshi hilo kuanzia April 16 hadi Mei mosi 2021.
Amesema mbali na Dawa za kulevya, pia wamekamata vyombo vya usafiri ambavyo ni magari nne na pikipiki tano, vilivyokuwa vikisafirisha mirungi na gari moja iliyokuwa ikisafirisha simu za magendo na kwamba vyombo hivyo vitataifishwa kwa mujibu wa sheria.
“Pia tumekamatwa Pombe haramu aina ya Gongo lita 223, mitambo 4, ya kutengeneza gongo, nyavu haramu za uvuvi (makokoro) 180 pamoja na simu za kiganjani 237 za aina mbalimbali, zilizoingizwa nchini kwa njia za magendo,” RPC Kilimanjaro