Waziri wa Kilimo Peter Munya nchini Kenya ameipokonya mamlaka Taasisi inayohusika na kutoa idhini ya kuingiza nafaka nchini Kenya (AFA) katika maeneo ya mpaka.
Munya amesema Serikali badala yake itaitumia Taasisi ya Ukaguzi wa usalama wa mazao (Kephis) kuhakikisha kuwa mahindi yana viwango vinavyohitajika.
“Kuanzia sasa, AFA haitasajili mahindi ambayo tayari yamesajiliwa na Kephis. Sisi sote tunahimiza kuchukuliwa sampuli moja wakati malori ya kampuni moja yanapoingiza bidhaa’’ Munya Ijumaa iliyopita wakati alipotembelea mpaka wa Namanga.
Hatua hiyo inafuatia agizo la wiki iliyopita la Rais Uhuru Kenyatta kwa Munya kuhakikisha idhini ya kuingiza mahindi inapatikana haraka wakati wa Ziara ya kiserikali ya siku mbili na Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu.
Kenya ilipiga marufuku mara moja ununuzi wa mahindi kutoka mataifa jirani ya Tanzania na Uganda.
Kulingana na barua iliyoandikwa na Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya kilimo na chakula, Kello Harsama kwa Pamela Ahago ambaye ni Kamishna wa forodha katika mamlaka ya ushuru nchini Kenya KRA, ununuzi huo ulisitishwa baada ya uchunguzi kubaini kwamba mahindi kutoka mataifa hayo mawili sio salama kwa matumizi ya chakula cha binadamu.