Mbio za Mwenge wa Uhuru zimezinduliwa katika Mkoa wa Kusini Unguja visiwani Zanzibar alipozaliwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na zitahitimishwa mkoani Geita wilaya ya Chato alipozaliwa Hayati John Magufuli, Rais wa awamu ya tano.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama
“Mbio za Mwenge mwaka huu ni maalumu, mtaona zilipozinduliwa ndipo alipozaliwa Mheshimiwa Rais Samia na zitahitimishwa Oktoba 14 wilayani Chato alipozaliwa hayati Magufuli,” Mhagama.
Naye Kaimu Waziri wizara ya Habari Vijana na Michezo, Leila Mohamed Musa amesema mwenge huo utakimbizwa katika wilaya 150 za kiutawala badala ya wilaya 195.
Amesema kupitia mbio hizo wananchi watabuni na kuanzisha miradi kwa ajili ya maendeleo na kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Tehama ni msingi wa Taifa endelevu itumike kwa usahihi’.