Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amekabidhiwa rasmi ofisi, leo May 23, 2021 na mtangulizi wake Humphrey Polepole ambaye kwa sasa ni Mbunge.
Makabidhiano hayo, yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba. Shaka amemshukuru Polepole kwa kutenga muda wake na kuja kumkabidhi ofisi na kumuahidi kuendelea kushirikiana naye muda wote.
Pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu, Shaka amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua na kumuamini katika nafasi hiyo adhimu,“Naomba niwasihi viongozi wote waliopewa mamlaka katika serikali na chama, kwamba; wanajukumu kubwa la kumsaidia Rais na Mwenyekiti wetu wa chama.”.
Akitilia mkazo jukumu la chama kukisimamia chama, Shaka amesema ni muhimu sana serikali kuhudumia wananchi wakati wote, “Wadau wetu wakubwa ni Watanzania, bila ya kujali vyama vyao, dini wala makabila yao.”
Akiongea awali, Polepole amesema; “Katika chama chetu, tuna utamaduni wa kuachiana vijiti. Leo, namkabidhi ndugu Shaka kijiti hiki akikimbize.”