Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda na Uwekezaji (SCTIFI) kwa ngazi ya wataalamu umeanza leo jijini Arusha ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa Mawaziri wa tarehe 28 Mei 2021.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo umetoa fursa kwa wataalamu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili utekelezaji wa maamuzi ya awali ya SCTIFI, ripoti ya Baraza la Mawaziri wa Fedha, ripoti ya Kamati ya Sekta ya Forodha na Ripoti ya Kamati ya Kisekta ya Biashara.
Mengine yaliyojadiliwa ni utekelezaji wa uamuzi wa mkutano juu ya EAC-EU EPA, ripoti ya kamati ya viwango ya Afrika Mashariki, ripoti kuhusu masuala ya ushindani, ripoti ya kamati ya sekta ya uwekezaji pamoja na biashara nyingine.
Aidha, Mkutano wa Baraza la Mawaziri kwa ngazi ya wataalamu utafanyika kuanzia leo (Jumatatu 24 hadi 26 Mei, 2021 na kufuatiwa na mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 27 Mei 2021 na baadae tarehe 28 Mei 2021 kufanyika mkutano wa Baraza la Mawaziri.
Mbali na mkutano wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la biashara, Viwanda na Uwekezaji (SCTIFI), pia Mkutano baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kenya utakaofanyika jijini Arusha, kuanzia 26 hadi 30 Mei, 2021 kwa lengo la kutatua Vikwazo vya Kibiashara.
Mkutano huu ni maelekezo ya Wakuu wa Nchi na Serikali katika ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoifanya nchini Kenya tarehe 04 hadi 05 Mei, 2021.
Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi wanachama sita ambazo ni Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.