Mkuu wa Majeshi nchini Tanzania (CDF), Jenerali Venance Mabeyo amehudhuria sherehe za kuagwa kwa mkuu majeshi wa Afrika ya Kusini, Jenerali Solly Zacharia Shoke zilizofanyika jana mjini Pretoria.
Kuhudhuria kwa sherehe hizo ni utaratibu uliowekwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kuimarisha ushirikiano wa diplomasia ya ulinzi.
Taarifa iliyotolewa na ubalozi wa Tanzania imeeleza kuwa Jenerali Mabeyo akiwa nchini humo ametembelea ubalozi wa Tanzania nchini humo na kupokelewa na Balozi Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
“Kwa kufuata miongozo ya sera ya mambo ya nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoelekeza kuendeleza diplomasia ya kisiasa na kutekeleza diplomasia ya uchumi,” imeeleza taarifa hiyo.
Balozi Milinzi alieleza kuwa hali ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona iliathiri eneo la uwakilishi na athari kubwa imeonekana katika uchumi kama nchi nyingine duniani zilivyoathirika.
“Mapema mwezi huu Afrika ya Kusini imeanza kuonyesha dalili za uchumi wake kutengamaa kutokana na sarafu yake kuimarika dhidi ya sarafu ya dola ya Marekani,” Milinzi
Kwa upande wa Jenerali Mabeyo ameeleza ziara yake Afrika Kusini imekuwa ya mafanikio na kuna mambo amejifunza.
Amebainisha kuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amelenga kuleta maendeleo ndani na nje ya nchi katika kutekeleza sera ya mambo ya nje ambapo mwelekeo unaelekeza kuimarisha diplomasia kwa kujenga mahusiano na nchi kwa kuimarisha diplomasia ya siasa na diplomasia ya uchumi.
“Ili malengo haya yafanikiwe kunahitajika kuwe na ushirikiano baina ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na taasisi nyingine zote ili kufanya utekelezaji wa diplomasia uendelee kuleta mafanikio sio tu kwa Serikali bali kwa wananchi wa Tanzania kwa ujumla,” Mabeyo