Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ametoa wito kwa waajiri nchini kutoa nafasi kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi kufanya mafunzo kwa vitendo kwenye maeneo yao ya kazi ili kuwaandaa kabla hawajapata soko la ajira.
Wito huo ameutoa Dodoma wakati akifunga Maonesho ya Pili ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi Prof.Ndalichako amesema kuwepo kwa ushirikiano kutaondoa changamoto kubwa wanayokutana nayo wamiliki wa vyuo ya kupata sehemu ya kuwezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo.
“Baadhi ya waajiri wamekuwa na mtazamo hasi na kukukataa kuwapokea wanafunzi kwa madai kuwa wanawapotezea muda kwa sababu wanaona kama bado hawajaiva hivyo naomba muone umuhimu wa kuwapatia nafasi ya mafunzo kwa vitendo na kuwafanyia tathimini kabla hawajamaliza .” Prof Ndalichako.
Amesema kupitia fursa ambazo zinatolewa na waajiri kama kutakuwa na mapungufu kwa wanafunzi wanaporudi vyuoni kabla ya kumaliza mafunzo yao vyuo vitachukua hatua za kurekebisha na italeta manufaa zaidi kwa waajiri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi NACTE John Kondoro, amesema kuwa kufanyika kwa maonesho haya kunasaidia kuchochea ustawi wa sekta ya elimu na mafunzo ya ufundi nchini na yamewezesha wananchi kuona mchango mkubwa unaotolewa na vyuo vya ufundi katika kuandaa raslimali watu itakayotumika katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mwalimu Josephat Maganga ameziomba taasisi zinazotoa mikopo kuona namna ya kutanua wigo wa kuwasaidia vijana wanaobuni vitu mbalimbali kuweza kupata mitaji.
Awali Katibu Mtendaji wa Baraza la Vyuo vya Ufundi Nchini (NACTE), Dkt.Adolf Rutayuga amesema kuwa maonyesho hayo yamekuwa na mwitikio mkubwa kwani mwaka huu Taasisi 151 zimeshiriki tofauti na mwaka 2019 ambapo Taasisi 139 zilishiriki.
Dkt.Rutayuga amesema kuwa takwimu inaonyesha kuwa jumla ya wananachi waliotembelea mabanda imeonyesha kuongezeka kutoka watu 14,500 mwaka 2019 hadi 14,730 mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Francis Nanai amesema sekta Binafsi imekuwa ikitoa nafasi za mafunzo kwa vitendo na itaendelea kupokea vijana wengi zaidi kujifunza kwa vitendo.
Aidha Nanai ameiomba serikali kuanzisha chombo cha juu cha kuratibu suala zima la kukuza na kuendeleza ujuzi nchini na pamoja na kulinda maslahi ya Taifa na ajira za vijana wa kitanzania kuangalia upya masharti ya vibali vya ajira za kazi.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Amani Kakana,ambaye ni mshindi wa jumla wa maonyesho, amesema hawatabweteka katika ushindi huo na wataendelea kuongeza juhudi kutatua changamoto katika jamii.
Maonesho ya Pili ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi yamefanika Jijini Dodoma kuanzia Mei 27 hadi Juni 2, 2021 na yameshirikisha Taasisi 151. Kauli mbiu ya Maonesho hayo ni “Kuimarisha Ushirikiano na Wadau katika Kukuza ujuzi kwa Maendeleo ya Viwanda”