Mhubiri na nabii wa Kimataifa kutoka Nchini Nigeria, Temitope Balogun Joshua, maarufu T.B Joshua amefariki Dunia usiku wa kuamkia leo.
Amefariki saa chache baada ya kumaliza Huduma katika Kanisa lake Jijini Lagos, TB Joshua ni mwanzilishi wa Kanisa la Synagogue Church of All Nation (SCOAN) na Kituo cha Televisheni cha Emmanuel
Taarifa iliyotolewa na kanisa lake la Scoan inaeleza kwamba TB Joshua alifariki muda mfupi baada ya kutoa huduma katika kanisa hilo Jumamosi.
“Jumamosi Nabii TB Joshua alizungumza katika mkutano wa washirika kupitia Emmanuel TV alisema ‘kila jambo na wakati wake, kuna wakati wa kuja hapa kwa maombi na wakati wa kurudi nyumbani baada ya ibada’.”
“Mungu amemuita nyumbani Nabii TB Joshua kwa mapenzi yake. Nyakati zake za mwisho hapa duniani alizitumia katika huduma ya Mungu. Hiki ndio kitu alichozaliwa kukifanya, alikiishi na kukifia,” inaeleza taarifa hiyo.
Enzi za uhai wake, TB alifanikiwa kutembelea Tanzania mwaka 2015 wakati wa mbio za uchaguzi mkuu zikiwa zimepamba moto.
Alifanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa mgombea wa CCM, Hayati John Magufuli.
TB Joshua aliingia kwenye msukosuko mwaka 2014 baada ya kanisa lake kuporomoka na kuua watu na wengine kujeruhiwa.
Mei 10, mwaka huu bintiye Sarah alifunga pingu za maisha na kijana wa Kitanzania Brian Moshi, jijini Arusha.
Alizaliwa Juni 12, mwaka 1963.