Treni mbili za abiria zimegongana nchini Pakistan mapema siku ya Jumatatu na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 30, huku wengine zaidi ya 100 wakijeruhiwa.
Treni moja, Millat Express ilitoka nje ya reli kabla ya kugongwa na treni nyingine, Sir Sayed Express. Haijafahamika mara moja kilichosababisha treni ya kwanza kuacha njia.
Wanakijiji wanajaribu kutoa miili ya watu kutoka katika mabaki ya treni hizo, takriban watu 15 hadi 20 wakiripotiwa kukwama.
Mkuu wa Polisi wa eneo hilo amesema kuwa zaidi ya watu 1,100 walikuwa ndani ya treni hizo mbili, huku ikidaiwa kuwa baadhi yao walikuwa wakisafiri kuhudhuria harusi.
Mamlaka za reli zimesema zimeagiza uchunguzi wa ajali hiyo wakati shughuli za uokoaji zikiendelea. Matukio ya ajali nchini Pakistan ni ya kawaida wakati serikali ikishindwa kuboresha miundombinu ya treni ambayo ipo katika hali mbaya.
Mwaka 1990, treni ya abiria ilitoka nje ya njia na kuigonga treni ya mizigo, na kusababisha vifo vya watu 210, katika ajali mbaya zaidi kutokea katika historia ya Pakistan.
WOSIA WA TB JOSHUA KUELEKEA BIRTHDAY YAKE “HAITAKUWA RAHISI, SITOWEZA KUSHEREHEKEA”