Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB Dkt. Adesina Akinumwi amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwa benki hiyo itaendelea kufadhili miradi ya maendeleo hapa nchini na ipo tayari kufadhili miradi mipya kwa kuwa Tanzania ina sifa za kuendelea kupata ufadhili.
Dkt. Adesina aliyepo Jijini Abidjan nchini Ivory Coast amesema hayo leo wakati akizungumza kwa njia simu na Rais Samia aliyepo Jijini Dar es Salaam kuhusu uhusiano wa Tanzania na benki hiyo ambayo imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.
Katika mazungumzo hayo Dkt. Adesina ambaye ameanza kwa kutoa pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kutoa pongezi kwa Rais Samia kwa kupokea kijiti cha Urais amesema Tanzania inafanya vizuri katika uchumi na ana matumaini makubwa kuwa Mhe. Rais Samia ataendeleza jitihada zilizokuwa zikifanywa na mtangulizi wake.
Ameahidi kuwa AfDB itatoa ufadhili kwa Tanzania ili kuanzisha benki za wajasiriamali zitakazowakopesha vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi stadi pamoja na kujihusisha na kilimo, jambo litakalosaidia kupungua kwa tatizo la ajira kwa vijana na kuwaongezea kipato.
Aidha, Dkt. Adesina amemualika Rais Samia kuhudhuria mkutano wa uwekezaji utakaowaleta wawekezaji wakubwa pamoja ambao unatarajiwa kuvutia mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuwekeza katika nchi mbalimbali.
Pia, Dkt. Adesina amesema AfDB imetenga dola za Marekani Bilioni 5 kwa ajili ya kusaidia wanawake na ameomba Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa uwezeshaji wanawake kiuchumi ambapo Mhe. Rais Samia amekubali ombi hilo.
Dkt. Adesina ameahidi kuleta wataalamu wa benki hiyo hapa nchini ili wakutane na wataalamu wa Tanzania kwa ajili ya kupitia miradi ambayo tayari inafadhiliwa na benki hiyo na kujadili fursa za kuanzisha miradi mipya.
Kwa upande wake Rais Samia amemshukuru Dkt. Adesina kwa salamu zake za pole na pongezi na amemshukuru kwa benki hiyo kufadhili miradi mingi ya maendeleo hapa nchini ikiwemo inayotekelezwa chini ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa awamu ya pili na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na benki hiyo.
Ameelezea kufurahishwa kwake na mradi wa AfDB wa kufadhili vijana wanaojihusisha na kilimo na wanaomaliza mafunzo katika vyuo vya ufundi stadi kwa kuwa ufadhili huo utawawezesha vijana wengi wa Tanzania kuzalisha mali.
Pamoja na kumpongeza Dkt. Adesina kwa ushindi wake wa kuchaguliwa kuwa Rais wa AfDB kwa kipindi cha pili, Mhe. Rais Samia amemuomba kuongeza nafasi za Watanzania wanaoajiriwa katika benki hiyo.