Nicole Harper (38) wa Arkansas Marekani amemshitaki Mahakamani Askari Polisi Rodney Dunn kwa kugonga gari lake na kusababisha likapinduka July mwaka 2020 wakati akiendesha kurudi nyumbani usiku.
Pamoja na Polisi huyo kujitetea kuwa alifanya hivyo baada ya kuona Nicole amekataa kutii amri ya kusimama haraka muda uleule aliotakiwa kusimama, Nicole amesema baada tu ya kupewa ishara ya kusimama aliwasha taa za ‘hazard’ kuashiria ametii amri lakini akaendelea kuendesha gari taratibu kutafuta sehemu salama ya kupaki kwani aliona sehemu aliyosimamishiwa haikua salama.
Wakati anatafuta sehemu salama ya kupaki Polisi huyo aliona amekaidi amri ya kusimama hivyo dakika mbili baadae akaamua kuligonga gari hilo kwa nyuma na kupelekea kuhama njia, kugonga kingo za barabara na kupinduka huku Nicole akiwa Mjamzito.
Baada ya kugundua kwamba Polisi alifanya kosa kisheria huku muongozo wa leseni za kuendesha gari Arkansas ukimpa Dereva haki ya kwenda kusimama sehemu anayoiona ni salama zaidi kwa wakati huo na kutakiwa tu kumuonesha Polisi ishara au kuwasha hazard kumpa ujumbe kwamba unatafuta sehemu salama ya kupaki, Nicole amemshitaki Mahakamani huku video iliyorekodiwa kwenye camera ya gari la Polisi ikitumika kama ushahidi.