Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua rasmi mpango wa tatu wa maendeleo ya taifa wa miaka mitano huku akiwahidi watanzania kuwa mambo yote yaliyoahidiwa katika kampeni za mwaka 2020 yatatekelezwa na mpango huo.
Majaliwa amezindua mpango huo leo June 29, 2021, jijini Dodoma akimuwakilisha Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango nakueleza kuwa fedha zitapopatikana na malengo ya mpango huo yatafikiwa kwa asilimia mia na zaidi.
“Nataka niwaahidi watanzania kwamba mambo yote tuliyowaahidi katika kampeni 2020 yanaendelea kutelekelezwa kupitia mpango huu na utekelezaji wa mpango wa tatu unatarajia kugharimu jumla ya shilingi trillion 114.8 “ Waziri Majaliwa.
Aidha, akielezea safari yake ya maendeleo Majaliwa amemshukuru Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kumuanzishia safari yake ya kisiasa.
“Nitumie nafasi hii kumshukuru Mhe. Jakaya Kikwete ndiye aliyenianzishia kufanya kazi utumishi ndani ya serikali, alinitoa darasani nakunipa ukuu wa wilaya kwa mara ya kwanza 2005, na nilipohudumu nikajikimbiza kwenda jimboni na kuwa mbunge, akaniteua kuwa Naibu Waziri wa Elimu nafasi niliyodumu kwa miaka 5, uwepo wangu hapa jukwaani na uwepo wake chini kwangu lazima niringie kwani ana mchango mkubwa katika maendeleo yangu,” Waziri Mkuu.
Hata hivyo katika kuhakikisha mpango huu unatelekezwa Waziri Mkuu ameziagiza taasisi za umma, idara zinazojitegemea, na wadau wote wa maendeleo kuhakikisha ofisi zao zote zina mpango huu ili kuwezesha utekelezaji kwa pamoja na viwango.