Kama unakumbuka mwaka jana kuna picha ilisambaa sana kutokea Kenya ikimuonesha Mwanaume kalala pembeni ya jeneza lenye mwili wa Marehemu Mke wake, taarifa ikufikie kwamba sasa Mahakama Kuu ya Meru Kenya imesema Polisi walikosea kufanya kitendo hicho cha kumzuia kusafirisha mwili huo hivyo alipwe fidia ya milioni 1.5 ya Kenya ambayo kwa Tanzania ni milioni 32.
Mwanaume huyo aitwae Charles Mwenda (32) wa Meru Kenya alizuiwa kusafirisha maiti ya Mke wake kwenda kuizika akitokea Malindi Pwani kwenda Meru akiwa na Waombolezaji wasiopungua 30 ambapo Polisi walimkatalia kuisafirisha kwa sababu muda wa Watu kusafiri ulikuwa umeisha kwa kuzingatia masharti ya kutotembea kutokana na corona.
Sasa Mahakama Kuu Meru imesema Mlalamikaji ambae ni Charles Mwenda anatakiwa kulipwa fidia na kwamba Polisi walitumia nguvu kupita kiasi walivyomkamata na kumpa mateso ikiwemo kunyeshewa na mvua kwa kulala na mwili wa Mke wake nje ya kituo cha Polisi na sasa Jaji Edward Muriithi amemuagiza Mkuu wa Polisi Kenya kuhakikisha Kijana huyo analipwa fidia na Jeshi la Polisi ndilo linatakiwa kutoa hizo pesa na kuwajibika kutokana na vitendo vyao vya uonevu.