Mahakama Kuu imekataa maombi ya kuzuia mchakato wa Uchaguzi wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuendelea ikiwemo maandalizi na kampeni wakati kesi ya msingi ikiendelea.
Uamuzi huo ulitolewa jana mbele ya Jaji Edwin Kakolaki baada ya kupitia hoja za pande zote mbili zinazopingana.
“Mlalamikaji anaomba zuio la muda la mchakato wa uchaguzi, katika hati yake ya kiapo alishindwa kuishawishi mahakama kukubali maombi yake, kutokana na hoja hiyo maombi ya zuio yamekataliwa, wajibu maombi watawasilisha majibu ya madai ya mlalamikaji Julai 6 na mlalakaji atawasilisha majibu kama yapo Julai 8 mwaka huu na kesi itaanza kusikilizwa Julai 9 mwaka.
Mawakili katika maombi ya kusimamisha kwa muda mchakato wa uchaguzi wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) walivutana vikali, mlalamikaji anataka zuio huku walalamikiwa wakiomba mchakato uendelee.
Mlalamikaji katika shauri hilo ni Ally Salehe na mlalakiwa ni Bodi ya Wadhamini ya TFF, TFF na Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi.
Wakili wa Mlalamikaji, Frank Chacha anaiomba mahakama kukubali maombi ya kusimamisha mchakato wote wa uchaguzi kwa muda wakisubiri usikilizwaji wa kesi ya msingi ya kusimamisha uchaguzi huo.