Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imetolea ufafanuzi wa fedha zaidi ya Tsh. Bilioni 600 zinazotozwa kwenye mitandao ya simu, namna zinavyokwenda kutekeleza miradi ya maendeleo, fedha hizi ambazo TAMISEMI wameongezewa kutoka Serikali Kuu zinatokana na tozo mbalimbali zinazotozwa kwenye mitandao ya simu kwa ujumla.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Ummy Mwalimu amesema fedha hizo zinakwenda kutekeleza miradi ya Elimu, Afya ya Msingi na miundombinu ya barabara.
Waziri Ummy amesema Tsh. Billion 125 zinatarajia kukamilisha maboma ya vyumba vya madarasa 10,000 ya Shule za Msingi na Sekondari, Billioni 200 kukamilisha maboma ya Zahanati 900 pamoja na vifaa tiba na Billioni 322 ujenzi wa Barabara na Madaraja.
Itakumbukwa kupitia Bajeti Kuu ya Serikali 2021, Waziri wa Fedha Dr. Mwigulu Nchemba alipendekeza kutoza Tsh. 10 hadi Tsh. 200 kwa siku kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio kwa Watumiaji na kusema hili litapelekea kuongeza mapato ya Serikali kiasi cha Tsh. Milioni 396,306.0.
Waziri Mwigulu pia alipendekeza kutoza tozo ya Tsh.10 hadi Tsh.10,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa na kusema kiasi cha tozo kinatofautiana kulingana na thamani ya muamala unaotumwa au kutolewa na kwamba hili litaongeza mapato ya Serikali Tsh. Mili. 1,254,406.14.