Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Ummy Mwalimu amewaagiza Makatibu Tawala wasaidizi wa Mikoa yote nchini kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kikamilifu kwa weledi kwa kuzishauri, kuzisimamia na kutoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa bila uoga ili waweze kutimiza majukumu yao kikamilifu.
Ametoa maagizo hayo leo katika kikao na Sekretarieti ya Mkoa wa Katavi kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya maendeleo katika maeneo ya afya ya msingi, elimu ya msingi na sekondari na miundombinu ya barabara pamoja na ukusanyaji wa mapato na matumizi katika Halmashauri katika Mkoa wa Katavi.
Waziri Ummy amesema Makatibu Tawala wasaidizi wa Mikoa ni wakubwa zaidi kuliko Wakurugenzi wa Halmashauri, hivyo wanawajibu wa kuhakikisha wanawasimamia na kuwapa maelekezo ili kuweza kutoa matokeo chanya katika utekelezaji wa majuku yao ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Ameendelea kusema kuwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wanawajibu kuzisimamia, kuzishauri na kutoa maelekezo kwa Halmashauri 184 ili Ofisi ya Rais-TAMISMI kuendelea kutafuta rasilimali watu, rasilimali fedha na kupanga mikakati ya maendeleo itakayotekelezwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Ninawaagiza kuhakikisha mnahoji kwa undani bajeti za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuangalia vipaombele vya Serikali ambavyo vinasaidia kutatua changamoto za wananchi lengo likiwa ni kuziwezesha hizi Halmashauri kuweza kutimiza majukumu yao” Waziri Ummy