Mbunge wa Muheza Hamisi Mwinjuma a.k.a Mwana FA ambae yupo Jimboni kwake, ameshiriki kwenye ujenzi wa madarasa mawili ya Shule ya msingi Kwamkabala, Madarasa haya yalikuwa miongoni mwa ahadi zake alizotoa kwa Wananchi wakati wa kampeni na alishawezesha kukamilika kwa darasa moja kwenye shule hiyo ambayo awali ilikuwa na vyumba vitatu tu vya madarasa ambapo iliwalazimu Wanafunzi wa darasa la nne kuhamia katika Shule ya Msingi Masuguru ili kuendelea na masomo yao.
Vilevile Mbunge Mwinjuma ameendelea na ziara ya kuwashukuru Wananchi kwenye Kata mbalimbali na kushirikiana na Wananchi kufanikisha mradi wa kupeleka maji kata ya Pande Darajani ambapo kwa sasa hatua iliyopo ni kulaza mabomba toka kwenye tanki lililopo Muheza (ya Jimbo la Tanga) kuelekea kijiji cha Darajani.
Kwenye muendelezo wa ziara yake Jimboni, Mwana FA amefanya mkutano wa shukrani kwenye kata ya Mbaramo na klutumia nafasi hiyo pia kuwapa mrejesho wa changamoto mbalimbali za Kata hiyo alizozishughulikia hadi kufikia leo, hizi ni ziara ambazo anazifanya kwa sasa Jimboni ili kusimamia utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kuhakikisha ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni zinakamilika kwa Wananchi wa Muheza.