SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amepigilia msumari kwenye tozo ya miamala katika simu kwa kudai bunge ndio limepitisha na wale ambao wanapinga wanatakiwa kutoa mawazo mbadala nini kifanyike huku akisisitiza lengo ni ifikapo 2025 Tanzania liwe Taifa tofauti katika suala la Maendeleo.
“Sisi pale Bunge tumekaa kufikiria sasa kama watumishi wenu namna gani tunaweza kumaliza baadhi ya mambo ili tusonge mbele tunataka ifikapo 2025 kisiwepo kijiji Tanzania nzima ambacho kitakosa Umeme ni lengo kubwa”– Spika Ndugai
“Tunataka kupeleka Maji vijiji vyote tuna uhaba mkubwa sana wa madawati, tuna uhaba mkubwa sana wa Zahanati, na tunataka 2025 kila kijiji kiwe na Zahanati haya ni malengo makubwa sana”- Spika wa Bunge
“Tunayafikia vipi haya malengo ndio maana sisi wabunge tukaamua kwamba tunakwenda kwenye miamala hasa ukinuna sawa ukifanyaje sawa tunakwenda tutatoza kakitu fulani katika miamala fedha inayopatikana sio kodi ya kawaida inakwenda katika mfuko maalumu na fedha ile itarudishwa kwa wananchi wenyewe kupitia Maji, Barabara, Zahanati”- Spika wa Bunge
“Hakuna atakaekuja kutujengea nchi hii na unaepinga haya tupe mbadala tunawezaje kufanya hapa tutapata wapi Fedha kwahiyo maamuzi haya tumeyafanya kwa nia njema kabisa kwamba 2025 tuwe ni taifa la tanzania ambalo ni tofauti Afrika nzima”- Spika wa Bunge
Ndugai ameyazungumza hayo leo katika kikao kazi cha viongozi wa mkoa na wilaya zote za mkoa wa Dodoma kilichoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka kwa ajili ya kujadili muelekeo wa maendeleo ya mkoa huo.