Kulingana na vyombo vya habari, Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump anajaribu kuzuia uchunguzi wa kamati ya bunge ambao unapaswa kubainisha chanzo cha uvamizi wa jengo la Bunge Capitol Hill uliofanywa mwanzoni mwa mwaka huu.
Magazeti ya “Washington Post” na “Politico” yanadai kwamba wamepokea barua kutoka kwa wakili inayosema kwamba washirika wa zamani wa Trump wanaombwa wasitoe ushahidi mbele ya kamati hiyo. Wafuasi wa Trump walilivamia jengo la Capitol Hill mnamo Januari 6. Watu watano waliuawa. Trump alishutumiwa kwa kuwachochea washambuliaji hao.
Halikadhalika Rais Joe Biden hapo jana alikataa ombi la Trump la kuzuia nyaraka zinazohusu shambulio hilo kuwasilishwa kwa kamati hiyo ya bunge inayofanya uchunguzi. Trump alitaka afanyiwe upendeleo na kupewa kinga kama kiongozi wa zamani wa nchi hiyo.